Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (VETA) imetakiwa kushirikiana na Kiwanda cha kutengeneza samani za ndani cha EDOSAMA cha Kinyerezi jijini Dar es salaam kwa lengo la kuwaandaa watanzania wengi zaidi wenye ujuzi umahiri katika stadi ya useremala kwa ajili ya soko la ajira nchini na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Mohamed Omar wakati wa ziara yake katika karakana za kiwanda hicho iliyolenga kujionea namna shughuli za useremala zinavyoendeshwa pamoja na matumizi ya mashine na teknolojia za kisasa zinazotumika kuandaa samani za aina mbalimbali.

Akizungumza na uongozi wa VETA na EDOSAMA wakati wa ziara hiyo, Dkt. Omar amesema, moja matakwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kukuza ushirikiano kati ya waajiri, wenye viwanda na vyuo vya elimu na mafunzo nchini ili kuhakikisha kwamba vijana wanapata ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, kuajiriwa, kuajiri wengine pamoja na kuendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Na sisi kama Wizara ya elimu na wasimamizi wakuu wa mpango huo, tumeona upo umihimu wa ushirikiano kati ya VETA wenye jukumu la kuzalisha vijana kupitia utoaji mafunzo ya ufundi stadi na EDOSAMA kama kituo cha uandaaji mafundi mahiri katika eneo la utengenezaji samani ili kuzalisha vijana wenye uwezo na weledi wa kushindana kwenye soko la ajira nchini na nje ya nchi,” amebainisha Dkt.Omar.
Akishukuru kwa ziara na wito huo wa Naibu Katibu Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Kasore amesema, Februari, 2026 , Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ilizindua mpango wa ushirikiano baina ya waajiri, wenye viwanda na vyuo vinavyotoa elimu na mafunzo ya ufundi stadi ili kuhakikisha Watanzania, hasa vijana wanapatiwa ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na kufanikisha kufikiwa kwa malengo mahsusi ya Dira 2050.

“Jukumu letu VETA ni kuhakikisha tunayaishi maono ya Serikali ya awamu ya sita kwa kutoa mafunzo yatakayowapa Watanzania ujuzi na kuwaandaa kushindana katika soko la ajira na kukidhi mahitaji ya wenye viwanda, waajiri na mabadiliko ya teknolojia pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazofanyika hapa nchini kupitia ushirikiano huu alioelekeza Naibu Katibu Mkuu,” amesema CPA Kasore.
Ameongeza kuwa ushirikiano na EDOSAMA utawezesha kuandaa mitaala itakayoendana na mahitaji ya soko la ajira, wakufunzi wenye uwezo wa kuandaa vijana wenye uwezo na ujuzi unaohitajika sokoni pamoja na kuboresha karakana, mitambo na mashine zinazotumiwa kujifunzia na kufundishia.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa EDOSAMA, Bw. Edward Saguda amesema sekta ya misitu ni sekta yenye mchango mdogo sana katika uchumi wa nchi yetu ikichangiwa asilimia 3.5 ya pato la taifa, lakini ikitazamwa kwa jicho la tofauti na serkiali inaweza kuchangia zaidi ya asilimia 10 ya mapato ya serikali na kutengeneza ajira nyingi zaidi nchini.
Saguda ameitaka VETA kuharakisha kuanzisha ushirikiano na EDOSAMA ili kuisaidia Serikali na Watanzania kunufaika na sekta hiyo.