Latest Posts

LISSU ASISITIZA KUNA KASORO VIELELEZO VYA MASHAHIDI POLISI

Baada ya upande wa mashtaka (Jamhuri) kuhitimisha zoezi la maswali ya dodoso kwa shahidi wa kwanza ambaye pia ni mshtakiwa katika kesi ya uhaini, Tundu Lissu leo asubuhi Agosti 28, 2026, Lissu alisimama na kuiomba Mahakama kufanya Maswali ya ufafanuzi (Re-Examination) ambapo aliruhusiwa baada ya mjadala wa dakika kadhaa za hoja za upande wa jamhuri za kutaka kufahamu atafanyaje hivyo ikiwa Lissu anajiwakilisha mwenyewe kisheria.

Lissu alieleza kuwa haki ya kufanyiwa maswali ya ufafanuzi ni ya kisheria chini ya Kifungu cha 156(1) cha Sheria ya Ushahidi na kwamba kujiwakilisha mwenyewe hakuwezi kumnyima haki hiyo. Ameongeza kuwa hofu ya Serikali kuhusu yeye kuibua mambo mapya haina msingi, kwani Serikali inayo haki ya kuweka mapingamizi wakati wowote atakapovuka mipaka.

Baada ya jopo la majaji kuruhusu mchakato huo uendelee, Lissu alisimama kizimbani na kuanza kushusha ufafanuzi mzito wa kisheria juu ya masuala mbalimbali yaliyoibuliwa wakati wa mahojiano ya dodoso, akijikita katika kubomoa hoja za serikali na kuweka kumbukumbu sawa.

Lissu alianza kwa kufafanua jibu lake la “siyo kweli” alilolitoa asubuhi ya leo kuhusu kama nia ya kutenda kosa inathibitishwa na tendo husika. Alieleza kuwa siyo makosa yote ambayo nia yake inathibitishwa na matendo, kwani kuna makosa mengine ambayo nia yake inathibitishwa tofauti na matendo yenyewe, na hasa katika kesi za uhaini, tafsiri ya nia ina umuhimu wa kipekee wa kisheria.

Wakati wa dodoso, Lissu alibanwa kuhusu sababu za kutokuleta mahakamani tuzo zake za kimataifa alizozitaja. Akifafanua jambo hilo, Lissu alirejea kanuni kuu za ushahidi wa jinai zinazobainisha kuwa mshtakiwa hana wajibu wowote wa kuthibitisha kuwa hana hatia; badala yake, mzigo mzima wa uthibitishaji wa mashtaka na hatia upo mikononi mwa upande wa mashtaka pekee.

Lissu aligusia pia suala la “Constructive Publication” lililoibuliwa na upande wa serikali kuhusu video ya Jambo TV. Alieleza kuwa kisheria, uchapishaji wa namna hiyo unaweza tu kutokea ikiwa mshitakiwa ana mamlaka au udhibiti (control) juu ya uchapishaji husika. Lissu alifafanua kuwa yeye hakuwa na udhibiti wowote juu ya waandishi wa habari waliokuwa wanarusha matukio hayo live.

Lissu alielezea mashahidi wa siri (wa kificho) kama P1, P2, na P3. Alifafanua kuwa mashahidi hao hawajulikani na mtu yeyote ikiwemo mahakama yenyewe na upande wa utetezi isipokuwa na mawakili wa serikali waliowaleta, jambo linalofanya ushahidi wao kutoaminika. Lissu aliwaita mashahidi hao kuwa ni “wahalifu” kwa sababu walikiri kwa maandishi na kwa mdomo mahakamani kuwa walipanga njama za kufanya vurugu, na sheria inawachukulia kama wahalifu pindi wanapokiri wenyewe vitendo hivyo vya jinai mbele ya mahakama.

Mwishoni mwa utetezi wake, Lissu alitumia vielelezo vya maandishi D1, D2, D5, D15, na D14 kuonesha jinsi maafisa wa polisi walivyokiuka sheria kwa “kujishuhudia wenyewe”. Kielelezo D1 (John Kaaya) alisema kina sehemu ya saini ya mtoa maelezo na afisa aliyeandika lakini iliandikwa na Kaaya na kujishuhudia mwenyewe badala ya kuandikwa na askari mwingine.

Amesema kielelezo D2 cha Shahidi PW3 kilisainiwa na mtu mmoja kama mtoa maelezo na shuhuda. Kielelezo D5 (PW6), saini ya mtoa maelezo na ya afisa zimepigwa saini moja iliyogusa pande zote. Kielelezo D15 (Amini Mahamba): Kila ukurasa una saini ya mtoa maelezo lakini saini ya afisa aliyeshuhudia utoaji maelezo haijajazwa kabisa.

Aidha ameeleza kuhusu kielelezo D14 (PW15 Koplo Amani Michael). Amesema huyu ndiye shahidi pekee wa polisi ambaye kielelezo chake kipo sahihi kisheria kwasababu kina saini mbili tofauti zilizothibitishwa vyema.

Baada ya kumalizika kwa maswali ya ufafanuzi (Re-examination), jopo la majaji liliafiki kukamilika kwa ushahidi wa Tundu Lissu na kuahirisha shauri hilo hadi saa nane kamili mchana wa leo ili kuruhusu shahidi wa pili wa upande wa utetezi kupanda kizimbani kuanza kutoa ushahidi wake.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!