Latest Posts

TAHADHARI YA EL NIÑO: SERIKALI YAZIAGIZA KAMATI ZA MAAFA KUANZIA NGAZI YA VIJIJI KUJIANDAA NA MVUA KUBWA ZA VULI

Serikali ya Tanzania imetoa agizo zito kwa Kamati za Maafa katika ngazi zote kuanzia ngazi ya vijiji, mikoa, hadi taifa kujipanga kikamilifu na kuchukua hatua za dharura kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa za El Niño zinazotarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Septemba na wiki ya kwanza ya Oktoba 2026.

Wito huo umetolewa bungeni jijini Dodoma leo Ijumaa, Septemba 4, 2026, na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, wakati akiwasilisha hoja ya kuahirisha Bunge la 13, Mkutano wa Nne, ambapo amewataka viongozi na watendaji wa maeneo yote hatarishi kuanza maandalizi mapema ili kuzuia na kupunguza maafa yanayoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli kwa mwaka 2026, unaoonesha uwepo wa hali ya El Niño itakayoambatana na mvua kubwa kuanzia mwishoni mwa Septemba, na kuendelea Oktoba hadi Desemba. Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi ya ukanda wa pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki, ukanda wa Ziwa Victoria, pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma

Serikali imetahadharisha kuwa vipindi vya mvua hizi kubwa vinaweza kuambatana na mafuriko na kusababisha madhara makubwa ya kiafya, kijamii, kiuchumi, uharibifu wa miundombinu, na upotevu wa mali za wananchi.

 

Maagizo Maalum kwa Kamati za Maafa na Idara za Miundombinu

Katika kukabiliana na tishio hili, Serikali imetoa maelekezo yafuatayo kwa mamlaka na idara zote husika:

Uimarishaji wa Kamati za Maafa: Kamati zote za maafa kuanzia ngazi ya vijiji, mikoa hadi taifa zinapaswa kujiweka katika hali ya utayari wa hali ya juu na kuandaa mipango ya utekelezaji inayozingatia Mpango wa Taifa wa Dharura wa kukabiliana na El Niño.

Tathmini ya Maeneo Hatarishi: Maeneo yote yanayoweza kukabiliwa na mafuriko yanapaswa kutambuliwa mapema, tathmini za vihatarishi zifanyike, na kuhakikisha kuwa vifaa vya uokoaji, huduma za dharura, na mifumo ya mawasiliano viko tayari wakati wote.

Kusafisha Mitaro na Makalavati: Idara na taasisi zinazohusika na miundombinu na usafi wa mazingira zimeagizwa kusafisha na kuimarisha mitaro na makalavati mapema ili kuzuia blockages zinazoweza kusababisha mafuriko hata wakati wa mvua za kawaida, pamoja na kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote.

 

Ufadhili wa Matengenezo ya Dharura

Ili kuongeza ufanisi katika urejeshaji wa miundombinu itakayoharibika, Serikali imetenga fedha maalum kwa ajili ya matengenezo ya dharura. Waziri Mkuu alibainisha kuwa fedha za maendeleo ya miundombinu sasa hivi zinapelekwa moja kwa moja kwenye mifuko husika ili kuepusha urasimu na kuhakikisha huduma zinarejea haraka katika hali ya kawaida pindi maafa yanapotokea

Serikali imetoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na tahadhari zinazotolewa na mamlaka rasmi ili kulinda usalama wao na wa mali zao kuelekea msimu huu wa mvua

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!