Latest Posts

UTAMBULISHO NI MSINGI WA UNDUGU, USALAMA NA UCHUMI WA KIDIJITALI-WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema utambulisho ni msingi muhimu wa undugu, usalama wa nchi na maendeleo ya kiuchumi, akisisitiza kuwa mtu anapokuwa na utambulisho rasmi huwa rahisi kupata huduma na kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Dkt. Nchemba amesema hayo leo Jumatano, Septemba 16, 2026, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Utambulisho Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano Mlimani City jijini Dar es Salaam.

“Utambulisho ni msingi wa kwanza wa undugu. Hata ndugu waliozaliwa tumbo moja, wasipotambuana watatengana; tunasema huyu ni ndugu yangu kwa sababu ya utambulisho,” amesema.

Amesema utambulisho rasmi unamwezesha mwananchi kufanya miamala ya kifedha, kupata mikopo na kushiriki kikamilifu katika uchumi rasmi na wa kidijitali, huku mifumo ya utambulisho ikiunganishwa na taasisi mbalimbali za huduma za kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kwa kusema kuwa, Serikali pia inaendelea kuchukua hatua za kulinda taarifa binafsi zinazokusanywa na Mamlaka ya Vitamvuliso vya Taifa (NIDA) dhidi ya matumizi yasiyo halali na uvujaji, huku ikiimarisha usajili katika maeneo ya mipakani kwa ajili ya usalama na utambuzi wa raia.

Vilevile amesema Septemba 16 imechaguliwa kwa kurejelea Lengo la 16.9 la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, linalolenga kuhakikisha kila mtu anapata utambulisho wa kisheria ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, amesema watu 27,520,835 wameshasajiliwa NIDA, huku 23,515,667 wakiwa wamepatiwa NIN na vitambulisho 21,526,635 vikiwa vimezalishwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, amesema taasisi hiyo inaendelea kuboresha mfumo wa utambulisho kwa kuunganisha taarifa na huduma mbalimbali, ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, bima ya afya, TIN, leseni ya udereva na kundi la damu.

Amesema maandalizi yanaendelea kuwawezesha watoto kupata NIN tangu wanapozaliwa kupitia ushirikiano kati ya NIDA na RITA, huku mradi wa majaribio ukitarajiwa kuanza Kiolo, Rungwe na Kusini Unguja.

Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema lugha ni sehemu muhimu ya utambulisho wa jamii na taifa, akisisitiza umuhimu wa Watanzania kulinda utamaduni na lugha yao.

Katika hatua nyingine, Chalamila amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa NIDA kwa hatua zilizofikiwa, akisema zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Dar es Salaam wamefanikiwa kupata vitambulisho vya Taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!