Latest Posts

MGODI WA NORTH MARA WAZINDUA MICHEZO KUIMARISHA MAHUSIANO NA VIJIJI 11

 

Mgodi wa dhahabu wa North Mara umezindua mashindano ya michezo kwa lengo la kuimarisha mahusiano Bora , mshikamano na ushirikiano kati ya mgodi huo na wananchi wa vijiji 11 vinavyouzunguka.

Uzinduzi wa michezo hiyo umefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ingwe, Nyamongo, ambapo viongozi mbalimbali wameeleza umuhimu wa michezo katika kujenga umoja, kudumisha amani na kuimarisha mahusiano baina ya jamii na mgodi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya  Meja Edward Gowele, ameushukuru uongozi wa Mgodi wa North Mara kwa kuanzisha mpango huo, akieleza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuwaunganisha wananchi na kujenga mahusiano mazuri.

Aidha, amewataka viongozi wa kimila kuendelea kushirikiana na jamii katika kusimamia amani, umoja na mahusiano mema kati ya wananchi na mgodi.

 

Amewataka vijana kuacha tabia ya kuvamia migodi, akisisitiza kuwa migodi hiyo ni sehemu muhimu ya uchumi inayochangia upatikanaji wa mapato kwa wananchi na Serikali, ambayo hutumika kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, amesema kuwa uzinduzi wa Wiki ya Mahusiano kwa sasa unalenga zaidi kuimarisha ushirikiano kati ya jamii hizo mbili katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, pamoja na kuhakikisha kuwa amani na usalama wa kila mtu vinalindwa bila kujali tofauti za dini, rangi au kabila.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), Rashid Bugomba, amesema kuwa baada ya uzinduzi huo, michezo hiyo itaendelea katika vijiji husika ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuimarisha ushirikiano wao.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa wananchi na uongozi wa mgodi kushirikiana katika kutafuta suluhisho la changamoto ya uvamizi katika eneo la mgodi ili shughuli za uzalishaji ziendelee kwa usalama na hivyo kuwezesha upatikanaji wa fedha za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Naye Meneja Mkuu wa mgodi huo  Stephen  Doyle amesisitiza kuwa michezo ina mchango mkubwa katika kukuza vipaji, kutoa fursa za ajira na kuongeza kipato kwa vijana.
Hata hivyo, amebainisha kuwa bado kuna changamoto ya uvamizi katika eneo la mgodi, huku akiwataka wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kukabiliana na hali.

Ameongeza kuwa fedha za CSR zinategemea shughuli za uzalishaji wa dhahabu, hivyo mgodi uko tayari kuendelea kushirikiana na jamii katika kutekeleza miradi yenye tija na manufaa kwa wananchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!