Latest Posts

MSIGWA: KUTOSHIRIKI KWA CHADEMA HAKUTAKWAMISHA MARIDHIANO, KATIBA MPYA SI MILIKI YA VYAMA VYA SIASA

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amebainisha kuwa mchakato wa maridhiano ya kitaifa na marekebisho ya Katiba utasonga mbele kwa maslahi ya taifa zima, huku akisisitiza kuwa kutoshiriki kwa chama cha CHADEMA au taasisi yoyote hakutakwamisha juhudi hizo za kuleta mshikamano nchini.

Msigwa ametoa kauli hiyo leo wakati wa mahojiano maalum ndani ya kipindi cha Kasri cha Crown FM, siku moja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akutane na kufanya mazungumzo na wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa Ikulu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili uundaji wa Tume ya Taifa ya Maridhiano na mwelekeo wa mchakato wa marekebisho ya Katiba.

Akiangazia kutokuwepo kwa chama cha CHADEMA katika mkutano huo wa Ikulu, Msigwa ameeleza kuwa chama hicho kilipewa mwaliko kama vilivyo vyama vingine, lakini kikachagua kutohudhuria. Amesisitiza kuwa ingawa Serikali ingetamani kila dau ashiriki, kushiriki kwenye maridhiano si jambo la shuruti na mkutano uliofanyika ulikuwa halali kikamilifu.

Msigwa ameonya dhidi ya dhana kwamba nchi haiwezi kufikia maridhiano kwa sababu tu kundi fulani au taasisi fulani imeamua kujitenga. Amebainisha kuwa mchakato wa maridhiano unalenga maslahi ya nchi nzima na si ya chama au taasisi moja.

“Itakuwa ni makosa sana tukidhani kwamba kama nchi haiwezi kuridhiana kwa sababu kuna kundi fulani ama taasisi fulani haikutaka kushiriki… tungetamani taasisi zote zishiriki kwa sababu hili jambo linafanyika kwa maslahi ya nchi nzima sio kwa maslahi ya taasisi moja… Tusingependa tuache mtu yeyote nyuma lakini mtu asipotaka kushiriki pia tutasonga mbele kwa sababu maridhiano lazima tuyafanye.” Ameeleza.

Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Msemaji Mkuu huyo wa Serikali alieleza kuwa Katiba si miliki ya vyama vya siasa, asasi za kiraia wala wanaharakati, bali ni mali ya Watanzania wote. Amekumbusha kuwa kundi kubwa la wananchi nchini si wanasiasa na wala haliko kwenye vyama vya siasa, hivyo mchakato huo utahakikisha makundi yote yanashirikishwa kikamilifu

“Sasa hivi tunapokwenda kuandika Katiba mpya, Katiba sio mali ya vyama vya siasa wala sio mali ya asasi za kiraia ama wanaharakati; Katiba ni mali ya Watanzania… Bahati mbaya watu wengi wanadhani Watanzania wote ni wanasiasa, actually kundi kubwa la Watanzania sio wanasiasa na hawako kwenye vyama vya siasa.” Ameeleza.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!