Watumishi wa sekta ya afya nchini wametakiwa kwenda kufanya kazi katika Halmashauri za pembezoni mwa nchi ili kupunguza uhaba wa wataalamu hao unaokadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 50.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema hayo Julai 29, 2024 wakati wa Kongamano la kumbukizi ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Upungufu huo unaovikabili vituo vya afya, zahanati na baadhi ya hospitali za Halmashauri umetajwa kuchangia kudhoofisha hali ya utoaji wa huduma za afya.
“Niwatoe hofu watumishi wa afya kutoogopa kufanya kazi katika maeneo ya pembezoni mwa nchi kwa kuwa huduma zote muhimu za kijamii zinapatikana ikiwamo umeme, barabara, maji pamoja na shule.” Amesema Waziri Ummy.
Aidha amesema mkutano huo utajadili masuala ya rasilimali watu kwenye sekta ya afya ambao ni uzalishaji wa wataalamu wa afya ndani ya nchi na ubora wa watumishi wa afya kwa kuhakikisha watumishi wanasalia kwenye maeneo waliyopangiwa kuhudumia wananchi.
Waziri Ummy amesema Hayati Rais Benjamini Mkapa alikua ni muumini na kinara kwa kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya ikiwamo Sheria ya Bima ya Afya ya NHIF aliyoiasisi Mwaka 2,000.
Waziri Ummy amesema hivi sasa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) umekuwa chanzo kikuu cha mapato yanayotokana na huduma zinazotolewa kupitia mfuko huo.
Kongamano hilo linakutanisha wadau mbalimbali katika Sekta ya Afya ambapo watajadili masuala mbalimbali kuhusu Sekta ya Afya na linatarajiwa kufunguliwa rasmi Jumanne Julai 30, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
Kinachotarajiwa pia ni maoni na ushauri wa wadau mbalimbali wa Sekta ya Afya ikiwamo Sekta binafsi katika kutengeneza mkakati wa Sita wa Taifa wa Sekta ya Afya Mwaka 2026/2031 ambao unaendana na kukamilisha Dira ya Taifa ya Mwaka 2050.