Latest Posts

HAMAS YAKATAA MPANGO WA MAREKANI WA KUSITISHA MAPIGANO GAZA

Afisa mwandamizi wa kundi la Hamas amethibitisha kwamba kundi hilo litakataa pendekezo jipya la Marekani la kusitisha mapigano huko Gaza, ambalo pia linahusisha kuachiliwa kwa mateka walioko mikononi mwa Hamas.

Taarifa hiyo inakuja huku Ikulu ya Marekani (White House) ikitangaza siku ya Alhamisi kuwa Israel tayari imeridhia mpango wa mjumbe wa Marekani, Steve Witkoff, na inasubiri jibu rasmi kutoka kwa Hamas.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, pendekezo hilo linajumuisha kuachiliwa kwa mateka 10 walio hai na miili ya mateka 18 waliokufa kwa awamu mbili. Hatua hiyo ingewezesha kusitishwa kwa mapigano kwa siku 60, pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina walioko gerezani Israel.

Hata hivyo, afisa huyo wa Hamas akizungumza na kituo cha habari cha BBC amesema kuwa pendekezo hilo halijajibu madai yao ya msingi, likiwemo kusitishwa kwa vita kabisa, na kwamba watalijibu kwa wakati muafaka.

Serikali ya Israel haijatoa kauli rasmi hadi sasa, lakini Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu anaripotiwa kuwaambia familia za mateka siku ya Alhamisi kwamba amekubali mpango huo wa Witkoff.

Tangu tarehe 18 Machi 2025, Israel iliweka vikwazo na kurejesha mashambulizi ya kijeshi Gaza baada ya kusambaratika kwa makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa miezi miwili, chini ya usimamizi wa Marekani, Qatar na Misri.

Taarifa za ujasusi wa Israel zinaonesha kuwa Hamas bado inawashikilia mateka 58, huku takribani 20 kati yao wakiaminika kuwa bado hai. Serikali ya Israel imesema kuwa shinikizo la kijeshi ni njia ya kuwalazimisha Hamas kuwaachilia mateka hao.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!