Na Vanessa Sindato.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, ameitaka serikali na vyombo vya utungaji sheria kubadilisha mfumo wa uchaguzi nchini, akieleza kuwa mabadiliko hayo ni muhimu kwa taifa kupata viongozi kwa njia ya haki na uwazi.
Akihojiwa hivi karibuni katika kipindi maalum cha Maswali na Majibu kinachorushwa na Jambo TV, Heche amedai kuwa baadhi ya vipengele vya sheria ya uchaguzi vinafanya wagombea wao kuenguliwa bila sababu za msingi, jambo linalokinzana na misingi ya demokrasia.
“Ukisoma kifungu cha 50 cha sheria ya uchaguzi kinaonesha kabisa kwamba wataenda kuengua wagombea, ukisoma kifungu cha 45 (7) kinazungumza jinsi ambavyo msimamizi wa uchaguzi anaweza kuamua akahama na matokeo akaenda kutangazia anapotaka”, amesema Heche.
Aidha Heche amedai Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupitia ibara ya 74 haioneshi tume huru kama inavyosema, bali inalinda walioko madarakani.
Vilevile, amesisitiza kuhusu kauli ya No Reforms, No Election kuwa ni msimamo wa msingi wa chama na wala si propaganda ya kisiasa. Ameongeza kuwa kauli hiyo ni wito wa mageuzi ya kweli ya mfumo wa uchaguzi akidai Watanzania wengi wanachukizwa na jinsi mambo yanavyoendeshwa na serikali.
“Watanzania wanaona watu wanatekwa, wanachukizwa na jinsi serikali inavyoendesha mambo. Wanakasirishwa na jinsi uchumi wao unavyochezewa. No Reforms No Elections si mchezomchezo, ni msimamo wa kubadilisha nchi,” amesema Heche.
Aidha Heche amekosoa kauli na mwelekeo wa serikali kuhusu ajenda ya 4R (Mabadiliko, Ustahimilivu, Maridhiano na Kujenga Upya) akidai kuwa ni mbinu iliyoigwa na Rais Samia kutoka kwa mwanamama Sheikh Hasina aliyekuwa Waziri Mkuu wa Bangladesh bila kuzingatia hali halisi ya wananchi wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Heche amehoji vikali sera na taratibu za serikali kuhusu umiliki wa ardhi na wawekezaji wa kigeni, hasa kutoka China, akisema Watanzania wanaumia kuona ardhi yao ikimilikiwa kwa kiwango kikubwa bila kufuata utaratibu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), mamlaka iliyoundwa hivi karibuni kupitia muunganiko wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Eneo Huru la Uwekezaji kwa Mauzo Nje (EPZA).
“Leo nchi hii Wachina wanakuja bila kupitia TIC, wanamiliki ardhi, hairuhusiwi mgeni kumiliki ardhi hapa labda mpaka uwe umepitia TIC kumiliki ardhi, ambapo utaratibu wa umiliki wake sio wa kudumu lakini Wachina wanaenda huko vijijini wananunua ardhi laki 2, laki 5, milioni, wanamiliki heka 2000, 3000, 4000 kwenye nchi hii, Watanzania wanaona hayo mambo na yanawachukiza”, amesema.