Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Yusuph Makamba, amesema amepokea kwa moyo mkunjufu na utulivu maamuzi ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kumuengua kwenye orodha ya wanachama wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge katika jimbo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Makamba amezungumza hayo siku ya Jumatano wakati akizungumza na waandishi wa habari wa walioshtukiza na kufika ofisini kwake kwa lengo la kupata kauli yake kuhusu hatua hiyo ya chama.
“Ninaipokea na kuitii kwa moyo mmoja uamuzi wa Kamati Kuu. Mimi ni mwanachama na kiongozi mtiifu wa Chama Cha Mapinduzi. Chama kina taratibu zake, na wajibu wangu ni kutii maamuzi ya vikao vyake,” amesema Makamba.
Ameeleza kuwa ameshawasiliana rasmi na uongozi wa CCM ngazi ya wilaya na kuwaarifu utayari wake wa kushirikiana nao pamoja na wanachama wengine kuhakikisha chama kinashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.
Akizungumzia taarifa zinazosambaa mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari kwamba sababu ya yeye kukatwa ni kutokana na madai kuwa anadaiwa kuwa na nia ya kugombea urais wa Tanzania, Makamba amekanusha vikali madai hayo, akisisitiza kuwa hana nia hiyo kwa sasa na kwamba hajawahi kuonesha dhamira hiyo.
“Mimi si mgombea wa urais, wala sijawahi kutangaza nia hiyo. Hayo ni maneno yanayozunguka kwenye medani za siasa. Kwenye siasa changamoto kama hizi ni za kawaida, na mimi niko tayari kuzipokea kwa heshima na utulivu,” amesema.
Kuhusu tetesi zinazodai kuwa huenda akahama chama kutokana na kukatwa katika mchakato huo, Makamba amekanusha uvumi huo akisema bado yupo ndani ya CCM na kwamba chama hicho bado kinabeba imani na maono yake ya kisiasa.
“Niko CCM, na niko sana. Chama hiki ndicho kilichonilea, kimenipa nafasi za kuwatumikia wananchi na bado naamini katika misingi yake. Sio kila changamoto ni sababu ya mtu kuhamahama,” amesisitiza.
Makamba aliwahi kuwa mbunge wa Bumbuli kwa vipindi vitatu na kushika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki na Waziri wa Nishati