Serikali ya Korea Kusini imeanza rasmi kuondoa vipaza sauti vilivyokuwa vikirusha matangazo ya kuipinga Korea Kaskazini katika mpaka baina ya nchi hizo mbili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza mvutano wa kisiasa na kijeshi. Taarifa hiyo imetolewa na Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini siku ya Jumatatu.
Kwa mujibu wa BBC, hatua hiyo inakuja chini ya serikali mpya inayoongozwa na Rais Lee Jae Myung, ambaye baada ya kuchukua madaraka mwezi Juni, alichukua hatua za haraka kusitisha matangazo ya propaganda yaliyokuwa yakimkosoa utawala wa Korea Kaskazini. Lengo kuu, kwa mujibu wa serikali ya Seoul, ni kufungua tena milango ya mazungumzo na Korea Kaskazini baada ya miaka kadhaa ya mahusiano yaliyogubikwa na mvutano na ukimya wa kidiplomasia.
“Kuondolewa kwa vipaza sauti ni hatua ya kivitendo ya kusaidia kupunguza mvutano kati ya Kusini na Kaskazini,” imeeleza Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Hata hivyo, pamoja na hatua hizi za upole kutoka Korea Kusini, Pyongyang haijaonesha utayari wa kujibu kwa mtazamo wa maelewano. Wiki chache zilizopita, Korea Kaskazini ilikataa pendekezo la kurejea katika meza ya mazungumzo, ikisema haina nia yoyote ya kuanzisha mazungumzo na Korea Kusini.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuwa ya baridi kwa muda mrefu, hasa tangu kumalizika kwa vita vya Korea vya mwaka 1950 hadi 1953, ambavyo vilifikia tamati kwa makubaliano ya kusitisha mapigano badala ya mkataba wa amani wa kudumu.