Latest Posts

MPANGO WA TRUMP WA GAZA WAZUA TAFRANI, AFRIKA MASHARIKI YATAJWA KUPANGWA KUWAPOKEA WAPALESTINA

Marekani na Israel zimefanya mawasiliano na maafisa wa serikali za mataifa matatu ya Afrika ikiwamo yale ya Afrika Mashariki ili kujadili uwezekano wa kutumia ardhi yao kama maeneo ya kuwahamishia Wapalestina watakaotolewa katika Ukanda wa Gaza chini ya mpango wa baada ya vita wa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Maafisa wa Marekani na Israel wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa mawasiliano hayo na Sudan, Somalia, na eneo la Somaliland ambalo limejitenga na Somalia yanaonesha azma ya Marekani na Israel kusukuma mbele mpango huo, licha ya kukosolewa vikali na kuzua masuala mazito ya kisheria na kimaadili.

Kwa kuwa maeneo hayo yote ni maskini, na mengine yanakumbwa na machafuko, pendekezo hili linaibua mashaka kuhusu lengo la Trump la kuwahamishia Wapalestina wa Gaza kwenye “eneo zuri.”

Maafisa wa Sudan wamesema wameukataa mpango huo, huku maafisa wa Somalia na Somaliland wakidai kuwa hawajafahamishwa kuhusu mazungumzo yoyote.

Katika mpango wa Trump, zaidi ya watu milioni mbili wa Gaza wangepelekwa sehemu nyingine ili wapate makazi ya kudumu. Amependekeza kuwa Marekani ichukue umiliki wa eneo hilo, kusimamia mchakato wa kulisafisha na kuliendeleza kama mradi wa ardhi.

Hapo awali, wazo la kuwahamisha kwa wingi Wapalestina lilizingatiwa kama ndoto ya kundi la kizalendo la mrengo mkali nchini Israel. Hata hivyo, tangu Trump alipolitoa wazo hilo katika mkutano wa Ikulu mwezi uliopita, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amelipongeza kama “dira yenye ujasiri.”

Wapalestina wa Gaza wameukataa mpango huo na wanakanusha madai ya Israel kwamba uhamisho huo ungekuwa wa hiari.

Nchi za Kiarabu zimeonesha upinzani mkali na kupendekeza mpango mbadala wa ujenzi upya ambao ungewabakisha Wapalestina katika ardhi yao. Makundi ya haki za binadamu yamesema kuwa kuwalazimisha au kuwashinikiza Wapalestina kuondoka kunaweza kuwa uhalifu wa kivita. Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imesisitiza kuwa Trump “anasimamia mtazamo wake.”

Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani na Israel waliokuwa wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina kutokana na usiri wa mpango huo wa kidiplomasia, mazungumzo na Somalia na Somaliland yamefanyika, huku Marekani ikithibitisha pia kuwa Sudan ilihusishwa. Hata hivyo, haijafahamika kiwango cha maendeleo ya mazungumzo hayo au ni viongozi wa ngazi gani walihusika.

Mawasiliano hayo ya Marekani na Israel na mataifa hayo matatu yalianza mwezi uliopita, siku chache baada ya Trump kuwasilisha mpango wake wa Gaza akiwa na Netanyahu. Marekani imeeleza kuwa Israel ndiyo inayoongoza mazungumzo hayo.

Israel na Marekani zina aina mbalimbali za motisha- kifedha, kidiplomasia, na kiusalama ambazo zinaweza kutolewa kwa washirika watakaokubali kushiriki katika mpango huo. Njia hiyo ni sawa na ile Trump alitumia miaka mitano iliyopita aliposimamia mkataba wa Abraham Accords, mkataba wa kidiplomasia kati ya Israel na mataifa manne ya Kiarabu.

Ofisi ya Netanyahu na Ron Dermer, waziri wa baraza la mawaziri la Israel na mshauri wa Netanyahu ambaye anaongoza mipango ya baada ya vita ya Israel, pia hazikutoa maoni.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha wa Israel, Bezalel Smotrich, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mtetezi wa kile anachokiita “uhamaji wa hiari” wa Wapalestina, amesema wiki hii kuwa Israel inafanya juhudi za kutafuta nchi zitakazowachukua Wapalestina. Amesema pia kuwa Israel inatengeneza “idara kubwa sana ya uhamaji” ndani ya Wizara ya Ulinzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!