Latest Posts

PROF. KITILA AVUTIWA NA UTENDAJI WA BANDARI YA DAR

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Raisi Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amepongeza uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na kampuni ya kimataifa ya uwekezaji ya DP World katika bandari ya Dar es Salaam na kuangalia ni namna gani serikali itaendelea na maboresho zaidi katika bandari hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwamo makusanyo ya kodi kupitia Dira ya Taifa ya miaka 25 ijayo (2050).

Akiongea wakati wa ziara yake ya kikazi bandarini hapo, Waziri Mkumbo amesema uwekezaji uliofanyika katika bandari ya Dar es Salaam ni mkubwa na una tija sana katika taifa katika maeneo mbalimbali ikiwamo ukusanyaji wa mapato na ufanisi mkubwa katika utoaji wa huduma na kuvutia wafanyabiashara zaidi kutumia bandari hiyo.

“Kiukweli nimefurahishwa sana na maboresho ya kimiundombinu na kiutendaji yaliyofanyika na haya ni matunda ya uwekezaji huu. Naipongeza sana menejimenti na uongozi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) kwa usimamizi mzuri na mipango mbalimbali inayoendelea katika upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam na bandari nyingine ili kukuza uchumi wa nchi,” amesema Waziri Mkumbo.

Amesema kupitia mipango ya Dira ya Taifa, Serikali inapenda kuona ni namna gani uwekezaji huu utazidi kuwa na tija katika miaka 25 ijayo kupitia mipango na mikakati mbalimbali ambayo Serikali imeipanga.

Amesema maboresho yanayoendelea kufanyika katika bandari hiyo kupitia uwekezaji uliofanyika yanachochea uwekezaji katika sekta mbalimbali hapa nchini kama vile sekta ya viwanda mbalimbali, sekta ya kilimo na sekta ya elimu, ambazo zote zitasaidia kuleta tija kwa nchi ikiwemo kutoa ajira na kukuza uchumi wa taifa.

“Namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu uwekezaji huu mkubwa na wa kihistoria kwa nchi yetu, kwani hivi sasa tumeanza kuona matunda yake” amesema Mkumbo.

Katika ziara hiyo Mkumbo amebainisha namna uwekezaji huo utakavyoweza kukuza uchumi hasa katika mipango ya nchi ya muda mfupi na mipango ya muda mrefu na kuona kuwa yana tija kwa pande zote mbili, akimaanisha upande wa serikali na upande wa muwekezaji.

Kampuni ya kimataifa ya DP World imepewa dhamana ya kuwekeza kwenye gati namba 4 mpaka 7, hivyo kusababisha kuongezeka kwa mapato baada ya maboresho mbalimbali ikiwamo meli kuweka gati na kupakua mizigo kwa muda mfupi sana tofauti na ilivyokuwa zamani.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!