Wananchi wa kijiji cha Ikombe kata ya Matema wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, wameitaka Serikali kuwatengenezea barabara kutokana na usafiri pekee wa majini wanaotumia katika ziwa Nyasa kutokuwa wa uhakika kwa sasa.
Wameeleza kwamba wakati mwingine wanashindwa kusafiri majini kutokana na dhoruba hivyo baadhi ya wagonjwa wanaohitaji huduma za dharula ikiwamo wajawazito hupoteza maisha.
Kufuatia hayo wameitaka serikali kujenga barabara ili kuwa na mbadala wa kusafiri badala ya kutegemea njia ya ziwani pekee.
Ikumbukwe tangu kuanzishwa kwa kijiji hicho mwaka 1976 hakijawahi kuwa na barabara hivyo wananchi hao wamepenyeza ombi kwa Serikali kupitia mbunge wao.
Mbunge wa jimbo la Kyela Ally Mlaghila amepokea ombi la wananchi wake na kueleza neema kwa wananchi hao (wa kijiji cha Ikombe) itakayosaidia kumaliza changamoto ya wanawake kujifungulia njiani wakielekea kutafuta huduma za kiafya.
Amesema Serikali itahakikisha inajenga barabara kwani tayari bajeti imetengwa ili kuwasaidia wananchi.