Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete anatarajiwa kuongoza harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya matibabu ya watoto 1,500 wenye matatizo mbalimbali ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Naibu Spika wa Bunge, Musa Azzan Zungu, wakati akizungumzia maandalizi ya harambee hiyo itakayofanyika tarehe 2 Novemba mwaka huu, katika Hoteli ya Rotana, Dar es Salaam.
Zungu alisema kuwa, takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa kati ya watoto 100 wanaozaliwa, wawili huwa na matatizo ya moyo. Hadi sasa, watoto 1,500 wamesajiliwa kwa ajili ya matibabu hayo, lakini hawana uwezo wa kugharamia matibabu.
Naibu Spika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Heart Team Africa Foundation, alisisitiza kuwa watoto hao wasipopata matibabu kwa wakati, wanaweza kupoteza maisha. Alitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kusaidia kwenye harambee hiyo ili kuchangia matibabu ya watoto.
“Nawaomba Watanzania tuungane kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuimarisha huduma za mama na mtoto. Serikali yake inachangia asilimia 70 ya gharama za matibabu kwa watoto wenye matatizo ya moyo, hivyo ni wakati mwafaka wa kumuunga mkono Rais wetu,” alisema Zungu.
Aliongeza kuwa watoto wengi wenye matatizo ya moyo wanatoka kwenye familia zisizo na uwezo, hivyo aliomba taasisi na mashirika mbalimbali kujitokeza kusaidia juhudi hizi.
JKCI, kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation, wameandaa harambee hii ili kukusanya asilimia 30 iliyosalia ya gharama za matibabu, sawa na shilingi milioni nne kwa kila mtoto.
“Nawaomba Watanzania wote, wafanyabiashara, taasisi binafsi na za umma, vilabu vya michezo, wasanii, mabalozi, na vyombo vya habari, tushiriki katika harambee hii yenye kaulimbiu ya ‘Tia Nuru, Gusa Moyo, Lete Matumaini kwa Watoto,’” aliongeza Zungu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya kwa kununua vifaa vya kisasa kwa hospitali zote kubwa nchini na kuwasomesha wataalamu wa afya.
Alibainisha kuwa madaktari bingwa wa JKCI wamejiandaa kutoa huduma bora za upasuaji kwa watoto na watu wazima watakaohitaji matibabu ya moyo katika taasisi hiyo.
“JKCI imeendelea kuwa hospitali kubwa na yenye vifaa vya kisasa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Mafanikio ya wagonjwa wanaopata tiba hapa ni makubwa, sawa na yale ya nchi zilizoendelea. Ndiyo maana madaktari bingwa duniani wanapenda kuja kufanya kazi na sisi,” alisema Dkt. Kisenge.
Aliongeza kuwa uboreshaji wa huduma za afya nchini umewavutia wagonjwa kutoka nchi mbalimbali kuja JKCI kwa matibabu ya kibingwa