Rais wa nchi ya Ukraine Volodymr Zelensky amesema kuwa zaidi ya makombora 100 na takribani ndege 100 za mashambulizi zilirushwa na Urusi usiku kucha zikilenga miundombinu muhimu ya kiraia katika mikoa mingi ya Ukraine, akitoa mfano wa mashambulizi dhidi ya miji ya Kharkiv, Kyiv, Odesa na maeneo ya magharibi.
Katika chapisho kwenye Telegram, Zelensky amesema kuwa kumekuwa na uharibifu mkubwa wa vifaa vya nishati ambavyo vinafanyiwa ukarabati huku akitoa wito kwa washirika wa Magharibi kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za masafa marefu na kuwaruhusu kupiga maeneo nchini Urusi ambayo mashambulizi yanaanzishwa.
Kulingana na taarifa ya Waziri Mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal, milipuko ilitanda katika miji kadhaa mikoa 15 huku takribani watu watatu wakiuawa.
“Tumeshuhudia kukatika kwa umeme huku mashambulizi ya Urusi yakilenga miundombinu ya nishati na maji. Wakazi wa Kyiv wanatafuta makazi katika vituo vya treni”, ameeleza Shmyhal.
Shambulio la Jumatatu ni shambulio la kwanza kubwa la Urusi kwa ndege zisizo na rubani na makombora tangu Kyiv ilipoanzisha uvamizi wake wa kushtukiza katika eneo la Kursk la Urusi mapema mwezi huu. Vikosi vya Ukraine vilichukua udhibiti wa makazi mengine mawili huko Kursk mwishoni mwa wiki, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema katika taarifa Jumapili jioni.
Poland ambayo ni nchi jirani na Ukraine nayo imeonekana kujizatiti ikimaarisha jeshi lake la anga kutokana na kuongezeka kwa shughuli za washambuliaji wa Urusi wanaoshambulia magharibi mwa Ukraine, ingawa Warsaw (Mji mkuu wa nchi ya Poland) bado inakataa kurusha makombora katika anga ya Ukraine.
Mara ya mwisho Poland kukusanya ndege zake za kijeshi ilikuwa wakati wa shambulio kubwa mnamo Julai 8, wakati Urusi iliposhambulia kwa bomu hospitali kubwa zaidi ya watoto huko Kyiv.