Maelfu ya wanajeshi wa Israeli wakiungwa mkono na helikopta, ndege zisizo na rubani, na magari ya kivita walivamia miji yenye migogoro ya Jenin na Tulkarm pamoja na maeneo mengine katika Ukingo wa Magharibi ulio chini ya utawala wa Israel mnamo Jumatano, na kuua Wapalestina wasiopungua 10.
Shambulio hili ambalo ni moja ya makubwa yaliyoshuhudiwa katika Ukingo wa Magharibi kwa miezi kadhaa, lilifuatia mfululizo wa uvamizi mdogo katika eneo hilo katika wiki za hivi karibuni huku vikosi vya Israeli vikijaribu kuangamiza makundi ya wapiganaji wa Kipalestina.
Wakati Israel, ikipambana na wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza na kukabiliana na ongezeko kubwa la mvutano na Hezbollah inayoungwa mkono na Iran katika Lebanon ya Kusini, operesheni ya Jumatano ilionesha hatari nyingi za usalama ambazo Israel imekuwa ikikabili tangu kuanza kwa vita vya Gaza mwaka jana.
Wizara ya Afya ya Kipalestina ilisema kuwa Wapalestina wasiopungua 10 walikuwa wameuawa katika maeneo tofauti ya Ukingo wa Magharibi na vikosi vya Israeli wakati wa operesheni hiyo.
Muda mfupi baada ya shambulio la awali, sauti za risasi na milipuko zilikuwa zikisikika kutoka kambi ya wakimbizi ya Jenin, mji uliojengwa kwa wingi ulio karibu na eneo kuu la jiji ambalo limekuwa eneo la shughuli za kigaidi kwa miaka mingi.
Msemaji wa kijeshi alisema operesheni ya Jumatano ilifuatia kuongezeka kwa shughuli za kigaidi katika miezi ya hivi karibuni, huku zaidi ya mashambulizi 150 kutoka Tulkarm na Jenin yakihusisha risasi au milipuko katika mwaka uliopita.
Alisema kuwa jeshi liliona kuwa kulikuwa na “hatari ya papo hapo” kwa raia lakini operesheni ilikuwa sehemu ya mkakati mpana wa kuzuia mashambulizi.
“Mzozo huu wa kigaidi katika eneo hili si mpya, haujaanza jana na hautaisha kesho,” alisema Luteni Kanali Nadav Shoshani katika mkutano wa waandishi wa habari.
Ukiachana na Jenin na Tulkarm, jeshi lilisema pia vikosi vilivamia Far’a karibu na Tubas katika Bonde la Jordan, na kuua angalau watu wanne katika shambulio la ndege zisizo na rubani.
Israel, ambayo inasema Iran inatoa silaha na msaada kwa makundi ya kigaidi, imeongeza operesheni zake, wakati walowezi wa Kiyahudi pia wameanzisha mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya jamii za Wapalestina.
Maelfu ya Wapalestina wanaeleza kuwa wamekamatwa katika uvamizi wa Israel na zaidi ya wapiganaji na raia 660 wameuawa katika Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki tangu vita vya Gaza kuanza karibu miezi 11 iliyopita, kulingana na takwimu za Wizara ya Afya ya Kipalestina.
Waisraeli wasiopungua 30 wameuawa katika mashambulizi mjini Jerusalem na Ukingo wa Magharibi katika kipindi hicho kulingana na takwimu za Israeli.
Vita ya karibuni kati ya Waisraeli na Wapalestina ulianza tarehe 7 Oktoba baada ya wapiganaji wa Hamas kuingia kutoka Gaza hadi kusini mwa Israel, wakiua 1,200 na kuchukua zaidi ya mateka 250 kulingana na takwimu za Israeli.
Mazungumzo ya kimataifa ili kumaliza mzozo huo yanaendelea, huku Hamas na Israel wakilaumiana kwa ukosefu wa maendeleo, na Marekani ikionesha matumaini kwamba mapatano yanaweza kufikiwa.