Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amepanda kizimbani kwa mara ya kwanza Jumanne katika kesi yake ya muda mrefu ya rushwa, akidai kwamba analengwa kwa sababu ya msimamo wake mkali kuhusu usalama wa taifa.
Â
Netanyahu, mwenye umri wa miaka 75, ndiye Waziri Mkuu wa kwanza aliyeko madarakani nchini Israel kushitakiwa kwa makosa ya jinai. Wakati huo huo, taifa lake linakabiliana na vita vinavyoendelea Gaza na changamoto mpya za kiusalama zinazoibuka katika kanda, ikiwemo Syria.
Â
Wiki iliyopita, majaji waliamua kuwa Netanyahu atoe ushahidi mara tatu kwa wiki, jambo linalomlazimu kugawanya muda wake kati ya mahakama na wizara ya ulinzi, ambazo ziko umbali mfupi kutoka mahakamani.
Â
Katika ushuhuda wake, Netanyahu amevishambulia vyombo vya habari vya Israel, akivilaumu kwa kuwa na msimamo wa mrengo wa kushoto na kudai kuwa vimekuwa vikimwandama kwa miaka mingi kwa sababu ya kupinga suluhisho la mataifa mawili.
Â
“Nimekuwa nikisubiri miaka minane kwa ajili ya fursa hii ya kusema ukweli,” alisema Netanyahu mbele ya mahakama yenye majaji watatu. “Lakini mimi pia ni Waziri Mkuu … Ninaongoza nchi kupitia vita vya pande saba. Naamini kazi hizi mbili zinaweza kufanyika sambamba.”
Â
Waendesha mashtaka wanamtuhumu Netanyahu kwa kutoa upendeleo wa kisheria wenye thamani ya takriban dola milioni 500 kwa kampuni ya Bezeq Telecom Israel.
Â
Anatuhumiwa pia kwa kujaribu kufanikisha mpango na mmiliki wa gazeti la Yedioth Ahronoth ili kupata habari nzuri kwa kubadilishana na sheria za kupunguza ukuaji wa gazeti pinzani. Netanyahu amekana mashtaka hayo na hajakiri kosa.
Â
Netanyahu amejitetea akisema, “Kama ningehitaji habari nzuri, ningehitaji tu kuashiria msaada wangu kwa suluhisho la mataifa mawili … Kama ningechukua hatua mbili kushoto, ningesifiwa.”
Â
Akiwa mahakamani, Netanyahu amejitokeza akiwa mwenye tabasamu na kujiamini, huku akiwasili mahakamani saa nne asubuhi. Kesi hiyo ilihamishiwa Tel Aviv kwa sababu za kiusalama na inafanyika katika chumba cha mahakama chini ya ardhi.
Â
Mawakili wake walidai kwamba uchunguzi dhidi yake ulikuwa na mapungufu ya msingi, wakisema kuwa “hawakuwa wakichunguza uhalifu, bali mtu binafsi.”
Â
Mapambano ya Netanyahu na sheria yamezua mgawanyiko mkubwa wa kisiasa nchini Israeli, huku mzozo wa sasa wa Gaza ukiwa umeondoa kwa muda kesi yake kutoka kwenye ajenda ya umma. Hata hivyo, kadri vita vinavyoendelea, mshikamano wa kisiasa umeanza kudhoofika.
Â
Mwezi uliopita, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu kwa madai ya uhalifu wa kivita katika mzozo wa Gaza, hatua inayoongeza changamoto za ndani na kimataifa kwake.