Latest Posts

RAIS KOREA KUSINI: NITAPIGANA HADI MWISHO LICHA YA TUHUMA ZA UASI

Rais wa Korea Kusini anayekabiliwa na mzozo wa kisiasa, Yoon Suk Yeol, ametetea uamuzi wake wa kushitukiza wa kutangaza sheria ya kijeshi wiki iliyopita, akisema kuwa hatua hiyo ilikuwa muhimu kwa kulinda demokrasia ya taifa hilo.

Katika hotuba ya kushtukiza iliyotangazwa moja kwa moja kupitia televisheni siku ya Alhamisi, Rais Yoon amesema kuwa alilazimika kuchukua hatua hiyo ili kuzuia kile alichokiita “kuporomoka kwa demokrasia” na kupambana na “udikteta wa bunge” unaodaiwa kufanywa na vyama vya upinzani.

“Ninajua kuwa hatua yangu imezua mjadala mkali, lakini ilikuwa ni uamuzi wa kisheria wa kulinda mfumo wetu wa kidemokrasia,” amesema Yoon.

Licha ya shinikizo kubwa la kumtaka ajiuzulu au afikishwe kwenye mchakato wa kumshtaki, Rais Yoon amesisitiza kuwa hatang’atuka madarakani. “Nitasimama kidete iwapo nitashtakiwa au kuchunguzwa. Nitapigana hadi mwisho,” ameongeza kwa msisitizo.

Rais Yoon na washirika wake wanakabiliwa na uchunguzi kuhusu mashtaka ya uasi, huku serikali ikitangaza marufuku ya kusafiri dhidi yake. Hata hivyo, Rais Yoon amekanusha tuhuma hizo, akieleza kuwa hatua yake ya kutangaza sheria ya kijeshi haikuwa uasi bali juhudi za kisheria za kulinda amani na utawala wa sheria. Aliwashutumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kutengeneza kile alichokiita “uchochezi wa uwongo” kwa lengo la kuiangusha serikali yake.

Katika hotuba yake, ambayo ni ya kwanza tangu alipotoa ombi la radhi kwa taifa siku ya Jumamosi, Yoon amesisitiza kuwa upinzani ni tishio kwa utulivu wa taifa. Amesema kuwa hatua yake ilikuwa inalenga kuulinda umma na kutetea demokrasia dhidi ya kile alichokitaja kuwa hujuma za kisiasa.

“Lazima tuwe na ujasiri wa kulinda taasisi zetu za kidemokrasia dhidi ya juhudi zozote za kuzidhoofisha. Hatua yangu ilikuwa kwa maslahi ya wananchi,” ameeleza Yoon.

Pamoja na kujitetea, Yoon ameongeza kuwa hataepuka majukumu yake ya kisheria na kisiasa. “Niko tayari kujibu maswali yote kuhusu hatua niliyofanya. Nitashirikiana kikamilifu na uchunguzi wowote utakaoanzishwa,” amesema Rais huyo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!