Katika mahojiano yake na Jarida la Time, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ameeleza kuwa Donald Trump ndiye kiongozi pekee ambaye Rais wa Urusi, Vladimir Putin, anamuogopa. Akiwa katikati ya mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoendelea nchini Saudi Arabia, Zelensky amefichua kuwa hatua kali za kidiplomasia zinazochukuliwa na Marekani zinaonekana kuathiri mtazamo wa Kremlin kuhusu vita hivyo.
Kwa mujibu wa Zelensky, wakati mmoja Marekani ilipotishia kuiwekea Urusi vikwazo vikali kwa kuendelea na mashambulizi yake ya mabomu, “Warusi waliogopa sana,” jambo lililoashiria kuwa msimamo mkali wa Marekani unaweza kuleta matokeo chanya katika mchakato wa amani. Rais wa Ukraine pia anaamini kuwa, kwa muda, Trump atatambua kuwa Putin si mtu wa kuaminika na kwamba ni dhaifu kuliko anavyoonekana.
“Ushindi wa Urusi katika vita hivi utakuwa balaa si tu kwa Ukraine, bali pia kwa Magharibi nzima, wakiwemo viongozi wa sasa wa Marekani,” amesema Zelensky, akionesha wasiwasi wake kuwa athari za kushindwa kwa Ukraine zitaathiri dunia nzima.
Akizungumzia msimamo wa Trump na timu yake, Zelensky anasema kuwa viongozi hao hawawezi kuruhusu kushindwa kwa Ukraine kwa sababu “wanaona jukumu lao katika historia” kama watu wenye ushawishi mkubwa ambao wanapaswa kuhakikisha vita vinafikia mwisho kwa heshima.
Mazungumzo ya amani kati ya Marekani, Ukraine, na Urusi yanaendelea, huku Marekani ikijaribu kusuluhisha mzozo huo kwa njia za kidiplomasia. Hata hivyo, bado kuna vikwazo vikubwa, ikiwa ni pamoja na msimamo wa Kremlin na masharti yanayopingwa na pande mbalimbali