Latest Posts

MBOGO AJA NA MPANGO MKALI KONDOA, ATAKA KIZAZI KIPYA CHA VIONGOZI UWT

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Jesca Mbogo, ametoa wito kwa wanawake wa Wilaya ya Kondoa kuhamasisha usajili wa wasichana katika Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ili kuhakikisha kizazi kipya cha viongozi kinaandaliwa mapema.

‎Akizungumza katika ziara yake ya kwanza wilayani humo tangu achaguliwe, Mbogo amesema ipo haja ya kuingiza wasichana wengi zaidi ndani ya jumuiya hiyo ili kuimarisha uhai na mustakabali wa UWT.

‎“Tumeendelea kubaki sisi wenyewe na umri unaenda. Nikirudi tena hapa, nataka nikute mmeingiza wasichana wengi zaidi. Nitaleta simu kwa ajili ya kuwasajili na tutashindana kata kwa kata kuona nani ataongoza kwa kuingiza wanachama wapya,” amesema Mbogo.

‎Amesisitiza kuwa malezi ya viongozi huanzia ngazi za chini, akieleza kuwa yeye mwenyewe alilelewa na wanawake waliomtangulia hadi kufikia nafasi ya uongozi aliyonayo sasa.

‎“Nilivyokuwa mdogo nililea na kuongozwa na wanawake waliotutangulia hadi nikawa kiongozi bora, sasa ni jukumu letu kuwalea wasichana wetu ili wawe viongozi bora wa kesho, hii jumuiya tutamuachia nani kama hatutawaandaa?” amehoji.

‎Achangia  ujenzi, atoa Wito wa Umoja

‎Katika kuunga mkono juhudi za maendeleo ya jumuiya hiyo, Mbogo alichangia mifuko 10 ya saruji pamoja na shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa jumuiya wilayani humo.

‎Mbali na masuala ya ujenzi, ametoa wito wa maridhiano miongoni mwa wanawake kufuatia kumalizika kwa uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kusameheana na kuanza upya kwa mshikamano.

‎“Naomba tusameheane. Hakuna aliyekuwa mkamilifu wakati wa uchaguzi. Kulikuwa na kusemana na kubishana, lakini sasa uchaguzi umekwisha, tubaki wanawake wa Kondoa na tuanze upya,” amesisitiza.

‎Aliongeza kuwa ushirikiano ni msingi wa maendeleo na kwamba bila maridhiano, utekelezaji wa majukumu hauwezi kufanyika kwa ufanisi.

‎Aunga Mkono Elimu ya Wasichana

‎Katika ziara hiyo, Mbogo alitembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana Kondoa, hatua aliyosema ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kusogeza mbele elimu ya mtoto wa kike.

‎Mbali na kukabidhi mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi, Mbunge huyo pia alishiriki zoezi la upandaji miti kuunga mkono kampeni ya “Dodoma ya Kijani” iliyoasisiwa na Rais Samia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!