Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa imeandika historia mpya ya utalii na uwekezaji baada ya mapema leo, Oktoba 31, 2026, kufikia kilele cha mbio za Kitonga Marathon 2026 zilizokusanya zaidi ya wanariadha 800.
Tamasha hilo lilihusisha ushindani mkali wa kilomita 5, 10, 21 pamoja na kupanda mlimani (Trail Run) zimehitimishwa na Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamad Chande.

Akihutubia umma Waziri Hamad Chande, ameeleza kuwa Mlima Kitonga kwa hapo awali ulihusishwa na ajali za barabarani, sasa unageuzwa kuwa fursa ya kiuchumi kupitia michezo na utalii wa asili.
Aidha Chande alizipongeza mamlaka kwa ubunifu huo, akisisitiza kuwa utajiri wa ardhi yenye rutuba, misitu, na hali ya hewa nzuri ya Kilolo ni kivutio tosha kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Atupele Fredy Mwakibete, amebainisha kuwa miundombinu mibovu na ukimya wa kutotangaza vivutio umekuwa kikwazo kikubwa kwa sekta hiyo, ambapo imepelekea watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Kilombero na Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa kupitia upande wa Morogoro badala ya Kilolo.
Kukabiliana na changamoto hiyo, Mwakibete ametangaza kuwa wilaya imetenga zaidi ya ekari 21,000 kwa ajili ya viwanda na kilimo cha kimkakati, huku akiwakaribisha wadau kuwekeza na kusaidia kuitangaza wilaya hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilolo, Siwema Jumaa, amefafanua kuwa mbio hizo zimeacha alama ya uhifadhi kwa kugawa mapipa 10 ya taka na mizinga 20 ya nyuki kwa vikundi vya vijana. Aidha, tamasha hilo lilijali jamii kwa kutoa misaada katika kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu cha Filipo kilichopo Image na Ilula.
Pia Siwema Jumaa amewakaribisha watalii kujionea utajiri wa vivutio vilivyopo wilayani humo ikiwemo Chui Camp, maporomoko ya maji ya Idenda na Uluti, mapango ya Magombelena, na Kaburi la kihistoria la Nyundo lililopo Lugalo ambalo limehifadhi kumbukumbu ya askari 300 wa Kijerumani.
Katika matokeo ya kilomita 21 (Half Marathon), Angelina Joseph kutoka Singida aliibuka kidedea kwa upande wa wanawake akifuatiwa na Dorcas Ilanda wa Arusha na Visa Mhalwa wa Iringa na kwa upande wa wanaume, nyota ya nguli Agustino Harry McAfee kutoka Babati, Manyara iling’ara baada ya kunyakua ushindi wa kwanza na kuhitimisha Kitonga Marathon 2026 kwa kishindo kikubwa.
