Latest Posts

“KATIBA KWANZA, KANUNI BAADAYE” MDEE AITAKA TUME KUTAMBUA MAMLAKA YA KATIBA

Mbunge wa Viti Maalum, Halima Mdee, amesema kuwa hoja za vyama vya upinzani hasa CHADEMA kuhusu kutosaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zina uzito mkubwa wa kisheria na kisiasa, akisisitiza kuwa hakuna kanuni inayoweza kuwa juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza kuhusu mzozo wa kisheria uliopo kati ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na CHADEMA, Mdee amesema ni jambo la kushangaza kwa nchi inayodai kuwa ya kidemokrasia kuruhusu mfumo ambapo chama kimoja kinakuwa na mamlaka yote huku vingine vikitegemea “huruma ya mshindani wao” kuweza kushiriki uchaguzi.

“Chama chochote makini cha siasa, ukienda kushiriki uchaguzi kwa kujifanya kipofu unajiangamiza mwenyewe. Na katika demokrasia ya kweli, vyama vyote vinapaswa kuwa sawa kwa mujibu wa sheria, si kutegemea huruma ya chama tawala ili kuingia bungeni,” amesema Mdee.

Ameeleza kuwa kisheria, Kanuni za Maadili ya Uchaguzi ni za daraja la chini, na haziwezi kupingana na Katiba wala Sheria ya Uchaguzi. “Kanuni ni kajukuu, au kakitukuu – huwezi kutunga kanuni ikawa juu ya Katiba. Hata kama kanuni ingesema asiyesaini hawezi kushiriki, hiyo haina nguvu ya kisheria,” amesisitiza.

Mdee pia amehoji uhalali wa Tume ya Uchaguzi kuwatangaza wasiotia saini kuwa hawana sifa ya kushiriki uchaguzi, akisema hiyo ni tafsiri ya kupotosha, hasa kwa kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachotoa mamlaka hayo kwa NEC.

“Sasa busara na ukomavu wa kisiasa ni kusikiliza hoja na kuzitafutia majibu. Wenye dhamana wana wanasheria na wataalamu, lakini lazima watumie busara na common sense kuona kwamba kuna tofauti kati ya mpini na makali. Serikali ina nguvu, iko chini ya CCM, na watu wa Tume wanatokana na huo mfumo. Ni wazi upinzani uko kwenye mazingira magumu,” amesema Mdee.

Kauli hiyo inakuja baada ya CHADEMA kutangaza kuzuia uchaguzi wa mwaka 2025 hadi pale mabadiliko ya sheria za uchaguzi yatakapofanyika, hatua ambayo imewafanya NEC kuwatangaza kuwa hawana sifa za kushiriki uchaguzi kwa kutosaini kanuni.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!