Hospitali moja mjini Goma imepokea zaidi ya majeruhi 200 tangu mapema Januari mwaka huu, kufuatia kuongezeka kwa mapigano kati ya jeshi la Congo na kundi la waasi la M23, Red Cross na vyanzo vya ndani vilisema Jumatatu.
Katika wiki za hivi karibuni, mashariki mwa Congo imekuwa uwanja wa mapigano makali kati ya jeshi la serikali na M23, kundi linaloungwa mkono na Rwanda. Kundi hilo limekaribia mji mkuu wa jimbo, Goma, na kusababisha ongezeko la idadi ya watu waliojeruhiwa, kulingana na taarifa za Red Cross.
“Tumeshuhudia ongezeko la watu waliojeruhiwa tangu mwanzo wa Januari,” alisema Myriam Favier, mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
“Kuanzia tarehe 1 hadi 21 Desemba tulihudumia wagonjwa 100, na kati ya tarehe 1 hadi 20 Januari tumekuwa na wagonjwa 211,” Favier aliongeza.
Siku ya Jumatatu, mapigano yalifikia milima ya Sake, mji ulioko takriban kilomita 20 magharibi mwa Goma, huku milipuko ikisikika kutoka Goma asubuhi, kwa mujibu wa waandishi wa AFP.
Tangu kuibuka tena mwishoni mwa mwaka 2021, M23, linalodai kulinda jamii ya Watutsi limechukua maeneo makubwa Mashariki mwa Congo, eneo tajiri kwa madini. Mapema Januari, M23 lilidhibiti Masisi, mji mkuu wa kiutawala wa wilaya ya Masisi, ulioko kilomita 80 kutoka Goma.
Jeshi la Congo limekuwa likijaribu kurejesha mji huo kupitia mashambulizi ya kupinga waasi, hali iliyosababisha wimbi jipya la watu kuhama makazi yao. Umoja wa Mataifa uliripoti Ijumaa kuwa zaidi ya watu 230,000 wamelazimika kukimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu, ikiitaja hali hiyo kuwa mojawapo ya “mizozo ya kibinadamu inayotia hofu zaidi duniani.”
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) liliomba tena kuheshimiwa kwa huduma za afya na vituo vya kibinadamu, baada ya wafanyakazi wake wawili kujeruhiwa kidogo kutokana na kombora lililogonga gereji ya shirika hilo karibu na hospitali ya Masisi. Kombora jingine liligonga choo kilichokuwa karibu na hospitali hiyo siku hiyo hiyo.
Chanzo cha usalama kiliiambia AFP kuwa mapigano ya sasa yana ukali usiowahi kushuhudiwa kwa miezi kadhaa, yakiwa na idadi kubwa ya vifo na matumizi ya silaha nzito.
Ripoti ya wataalamu iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi Julai ilieleza kuwa wanajeshi 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda walikuwa wakipigana bega kwa bega na waasi wa M23, huku Kigali ikisemekana kuwa na “udhibiti wa moja kwa moja” wa operesheni za kundi hilo.